Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (mwenye koti jeusi katikati)
akiwa na baadhi ya Mawaziri, Wabunge na Viongozi wa mkoa wa Tanga wakishiriki
kuifungua rasmi barabara ya Handeni – Mkata na Handeni - Korogwe huko mkoani
Tanga.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (aliyenyoosha mkono)
akifurahia jambo na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
anayempongeza kiongozi wa kikundi cha ngoma ya Selo baada ya kutumbuiza wakati
wa sherehe za ufunguzi wa barabara ya Mkata – Handeni - Korogwe. Anayeangalia
(kulia) ni Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Handeni Dkt. Abdallah Kigoda.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa tatu kutoka kushoto) akiwa
na baadhi ya Mawaziri, Wabunge na Viongozi wa mkoa wa Tanga wakishiriki kukata
utepe kuifungua rasmi barabara ya Handeni – Mkata na Handeni - Korogwe huko
mkoani Tanga.
Sehemu ya barabara ya Handeni – Mkata.
RAIS KIKWETE AZIFUNGUA BARABARA ZA MKATA – HANDENI NA
KOROGWE – HANDENI MKOANI TANGA.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amewataka wakazi wa Handeni na maeneo inakopita barabara ya Mkata – Handeni na
Korogwe – Handeni kutumia ipasavyo fursa ya kupatikana kwa barabara hizo za
lami kuyaboresha maisha yao.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo wakati wa sherehe za ufunguzi wa barabara inayoinganisha Makao Makuu ya Wilaya ya
Handeni na barabara kuu ya Tanga - Dar es Salaam kupitia Mkata na upande
mwingine kuunganisha na barabara kuu ya Tanga – Moshi – Arusha kwa upande wa
Korogwe.
Mhe. Rais ameelezea kuwa lengo la Serikali ni kuona kwamba, barabara ya
Mkata hadi Handeni inaendelezwa hadi Kondoa kupitia Kiberashi kwani kufunguka
kwa ukanda huu kutakuwa ni chachu kubwa ya kuinua shughuli nyingi za kiuchumi
hasa kwa sekta ya kilimo katika maeneo hayo inakopita barabara hiyo.
Akiwasilisha tarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS) Eng. Patrick Mfugale alielezea kuwa barabara ya
Mkata - Handeni ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami ina urefu wa kilometa 53.2
ikiwa imejengwa na Mkandarasi Sinohydro
Corporation Ltd kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama ya Shilingi bilioni
57.3. Eng. Mfugale alibainisha kuwa mkataba
wa mradi huu ulisainiwa mwezi June 2009 na kazi zikakammilika mwezi Novemba
2012 baada kutatua changamoto ambazo zilikuwa zinakwamisha kukamilika kwa
muradi huo mapema zaidi kama ilivyokuwa imepangwa kimkataba.
Ufunguzi wa barabara hiyo umeenda sambamba na ufunguzi wa barabara ya Korogwe
hadi Handeni ambayo vile vile imekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
Akitoa tarifa kuhusu miradi huo wa Korogwe – Handeni, Mtendaji Mkuu wa TANROADS
Eng. Patrick Mfugale alielezea kuwa Mkandarasi Sinohydro Corporation Ltd ndiye pia
iliyeijenga barabara hiyo ambayo ina urefu wa kilometa 65. Mkataba wa Mradi huu ulisainiwa mwezi June 2009 na
kazi zikakamilika mwezi June 2013 na imejengwa kwa ghrama ya Shilingi bilioni
63.2. Kiasi cha Shilingi bilioni 3.3 kimelipwa kama fidia kwa wale waliofuatwa
na barabara hiyo katika baadhi ya maeneo.
Naye Waziri wa
Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akielezea baadhi ya faida zitakazopatikana
kutokana na kujengwa kwa barabara hizo alibainisha kuwa barabara ya kutokea
Korogwe hadi Handeni ndiyo barabara itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano
wa magari katika barabara kuu ya TANZAM hasa
kwa wasafiri na wasafirishaji wanaotokea maeneo ya Iringa, Mikumi na mengineyo
katika ukanda huo.
Waziri
Magufuli alifafanua kwa kwa kupitia Mikumi, Kilosa, Turiani, Mziha hadi Handeni
na kuelekea Korogwe au Mkata mkoani Tanga kunapunguza zaidi ya kilometa 120
tofauti na kuzungukia Morogoro na Chalenze.
“Hivi sasa mtu
anayetokea Iringa analazimika kupitia Mikumi na Morogoro mjini hadi Chalinze
ndipo aelekee Tanga, mzunguko ambao ni mrefu kulinganisha na barabara hii ya
kupitia Mikumi, Kilosa Magole, Mziha hadi Handeni” alisistiza Waziri Magufuli.
Kwa upande
mwingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
aliwafahamisha wananchi waliohudhuria kwa wingi katika sherehe hizo kuwa,
tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika kwa barabara inayoanzia
Handeni kuelekea Kiberashi hadi Kwamtoro mkoani Dodoma.
Rais Kiwete aliabinisha
kuwa hatua hiyo pia imefikiwa kwa barabara ya Handeni, Mziha, Dumila, Kilosa
hadi Mikumi. “Hatua inayofuata ni kutafuta fedha za kujenga maeneo katika
sehemu hizo ambayo bado hayajapata makandarasi” alifafanua zaidi Rais Kikwete.
Hata hivyo Mhe. Kikwete alitumia fursa
hiyo kuwaasa wasafirishaji kuzingatia masuala ya usalama barabarani kwa kupakia
mizigo kulingana na viwango vilivyowekwa kisheria. Alielezea kuwa moja ya adui
wakuu waharibifu wa barabara ni uzidishaji wa mizigo kupita viwango vilivyowekwa
kisheria.
0 comments: