Abiria treni ya Dar walia hujuma TRL

ABIRIA waliosafiri na treni kutoka Ubungo Maziwa hadi Stesheni ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) Dar es Salaam, juzi walilazimika kuisubiri kwa saa mbili kutokana na huduma hiyo kusuasua huku ratiba ya kuondoka ikiwa haieleweki.
Hali hiyo ilitokana na ratiba ya treni kutofuatwa na kusababisha abiria waliozoea usafiri huo kurundikana huku kukiwa na sintofahamu juu ya hatima yao.
Wakizungumza na Tanzania Daima, baadhi ya abiria wa treni hiyo waliushutumu uongozi wa TRL na kudai kuwa wanamhujumu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kwa kufanya mambo ya makusudi na kumtaka waziri huyo kulitupia macho suala hilo.
“Hizi ni hujuma, watu wanajua treni halifanyi kazi toka saa tano kwanini wasirekebishe na hata kuunga vichwa mapema ili watu wakija saa 10 jioni waondoke? Lakini wao wakifika muda huo sababu kibao,” alisema mmoja wa abiria hao.
Kwamba wafanyakazi wa TRL waliendelea kukata tiketi kwa abiria licha ya kufahamu kuwa treni haiondoki kwa wakati na tangazo la kuhairisha safari ya treni hiyo iliyokuwa iondoke saa 10 jioni lilitolewa saa 10:15.
Hivi karibuni, Ofisa Habari wa TRL, Midladjy Maez, alikaririwa akisema mabadiliko ya safari za treni jijini yametokana na ubovu wa vichwa vya treni hiyo.
“Hii ni dharura na si kweli kama kuna mabadiliko ya ratiba… hakuna hujuma zozote, changamoto yetu ni hitilafu katika vichwa hivyo,” alisema Maez.

Chanzo: Tanzania Daima

Author

Written by DK

Napenda kusafiri, hasa kutembelea kila mkoa katika nchi yangu nzuri Tanzania, nafanya hivyo maana hiyo ndio njia niliyochukua katika kutumikia taaluma yangu ya habari na mawasiliano ya umma

0 comments: