Mohammed Mpinga Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani,Taifa.
Hospitali teule ya rufaa ya Tumbi iliyoko mkoani Pwani inabeba mzigo wa kutibu abiria majeruhi na kuwaunganisha na familia zao kila ajali zinapotokea.
Jukumu la kuwaunganisha na jamaa zao linatokana na mazoea ya uporaji yaliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa kila ajali inapotokea cha kwanza ni kuwaibia wasafiri kila wanalicho nacho kabla ya kuwasaidia.
Mganga Mkuu wa Tumbi, Dk Peter Dattan, anasema katika mahojiano kuhusu changamoto zinazoikumba hospitali hiyo inayoshughulikia asilimia nane ya majeruhi wote nchini.
Japo hakusema moja kwa moja kuwa inabidi watoa huduma kutumia simu zao na kuwasiliana na jamaa wa majeruhi ukweli ni kwamba hicho ndicho wanachofanya na wakati mwingine mhudumu wa afya analazimika kutoa nauli kusaidia wasafiri majeruhi wasio na msaada kurudi makwao.
Lakini tatizo la hospitali ya rufaa ya Tumbi kubeba mzigo wa huu umefika wakati wa kulipatia ufumbuzi, anasema Mganga Mkuu na kushauri kuwa wasafirishaji wa abiria na shehena magari yao yana bima hivyo bima zitumiwe kutibu na kuhudumia wasafiri wanaopata ajali.
“Fikiria basi la abiria 65 linapopata ajali unaletewa watu wote hapa Tumbi ambao bahati mbaya wameibiwa kila kitu fedha, simu na mizigo wakifikishwa hapa hawana kitu kadi za bima ya afya za benki zote zimeporwa unawasaidiaje? Anahoji Dk Dattan.
Anaeleza kuwa kazi kubwa ni kuokoa maisha hivyo wanaanza kuwatibu kila mmoja anahudumiwa kwa dawa, vifaa na rasilimali zinaelekezwa kuokoa maisha.
Baada ya tiba ni lazima huduma zilipiwe gharama za kila majeruhi hupelekwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili serikali ilipie matibabu hayo.
“Ikifikishwa wizarani tunatarajia serikali irudishe gharama hizo kwa kutupa fedha lakini hazirudishwi, wizara haitoi fedha wala vifaa hali inayosababisha wagonjwa wa kawaida wanapofika Tumbi wanakuta hakuna dawa, vifaa na kwa ujumla uendeshaji unazorota,” anasema Mganga Mkuu.
Ufumbuzi
Anataja mifano kuwa katika nchi nyingine abiria aliye ndani ya basi amelipiwa bima ya usafiri na maisha.Msafiri akipata ajali anagharamiwa na makampuni ya bima yanayohusika ambayo yana wajibu wa kuwahudumia majeruhi pia.
“Ili kuipunguzia Tumbi mzigo huu, serikali isimamie haya mabasi yalipe gharama za fidia na tiba. Basi ambalo linafanyabiashara abiria akilipia kiti pengine Sh 40,000 kiasi kadhaa mfano Sh 500 kielezwe kuwa ni kuchangia bima ya maisha ya msafiri.
“Hii iwekwe wazi ili wasafiri wafahamu kuwa kwenye gari kuna bima walizojigharamia zinazohusika na fidia na tiba pia.”
Anasisitiza kuwa ni jukumu la serikali kuanzisha mchakato wa kuwa na sera na sheria hizo na kwamba uongozi wa Tumbi umependekeza mara kuanza utaratibu huo na unasisitiza kuwa ni wakati wa utekelezaji.
Anashauri Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini na Nchikavu (Sumatra), chama cha wamiliki wa mabasi ya abiria (Taboa) na kampuni za bima kujadiliana na kutoa mapendekezo ya ushiriki wao.
Lengo ni kuona kuwa serikali kwa miaka mingi imewahudumia majeruhi wa ajali lakini pia ni lazima kungalia mbele ili kuamua namna ya kuwasaidia wasafiri wanaopata ajali kwa ufanisi hata ikibidi kuwakodishia watu helkopta kuwafikisha kwenye huduma za juu ili kuokoa maisha.
“Ifike wakati wananchi waelewe kuwa serikali haiwezi tena kuendelea kuchukua mizigo inabidi wadau hasa kampuni za bima washirikiane kuhudumia wasafiri majeruhi wa ajali”
Dokta Dattan anasema licha ya kuwa kituo cha kuhudumia majeruhi wa ajali bajeti inayokuja kwa hospitali hiyo ni ndogo na mara nyingi hawapewi fedha za fungu la matumizi mengine (OC) ambalo linahusu dawa, haki za wafanyakazi, gharama za maji na umeme .
Anaeleza kuwa kukosekana OC kulitokana na suala la umiliki wa hospitali hiyo ambayo awali imeanzishwa na ya Shirika la Elimu Kibaha, hata hivyo utata huo umemalizika na itawekwa chini ya mkoa wa Pwani.
Kuzorota huduma
Kuelekeza rasilimali nyingi kwenye kuhudumia majeruhi kunaathiri utoaji huduma hospitalini Tumbi kwa vile hadi sasa hospitali inadai madeni mengi na pia inadaiwa na wazabuni mbalimbali hali inayosababisha utoaji huduma kuzorota.
“Bajeti ya hospitali yetu ni sawa naya hospitali nyingine za rufaa mikoani. Sisi tuna wastani wa ajali tano kila siku, tunapata fedha sawa na hospitali ya Rufaa ya Maweni Kigoma ambayo inaweza pengine isipokee waathirika wa ajali. Lakini bajeti zetu zinafanana.”
Anasema deni lao ni kubwa wanadaiwa zaidi ya Shilingi bilioni na wazabuni mbalimbali wakiwamo waliowaletea dawa, waliotoa huduma za vyakula kwa wagonjwa lakini nao pia wanaidai serikali bilioni kadhaa.
Wataalamu/vifaa
Dokta Dattan anasema licha ya kuhudumia idadi kubwa ya majeruhi wanaopata ajali kuanzia Segera mkoani Tanga na wengine kutoka Bwawani mkoani Morogor o hadi Kibaha hospitali ina uhaba mkubwa wa wataalamu na vifaa.
“Tunahitaji wafanyakazi 687 lakini hali ilivyo idadi yao ni pungufu ya nusu wapo 290. Hakuna mtaalamu wa radiolojia,fizishani wa kutibu viungo vya ndani moyo, kisukari” anasema.
Anafafanua kuwa iwapo kutakuwa na wagonjwa wenye kuhitaji kusomewa taarifa za x-ray za magonjwa makubwa wanalazimika kuwatumia maradiolojia wa Dar es Salaam.
Anasema hospitali hiyo haina mtaalamu wa idara ya masikio, pua na koo (ENT) na hospitalini hakuna huduma hizo na kwamba maabara ya ENT haina vifaa.
Anataja mfano wa vyombo kama, taa mashine, wauguzi maalumu, dawa za usingizi kwa ajili ya chumba cha upasuaji na kwamba ili kukamilisha ujenzi wake zinahitajika Sh bilioni 10 kumalizia kazi hiyo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments: