Wema hauozi: Ajali ya mwaka 1979 na matokeo yake mwaka 1996


CHUKUA DK 7 KUSOMA
ITAKUJENGA NA KUKUSAIDIA
KIFIKRA NA MAWAZO WEMA
HAUOZI


 "Ni siku nyingi kidogo,
mwaka
1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma sana. Ilikuwa vigumu
sana kulisahau na lilinifanya
nijiulize, inakuwaje Mungu
anakuwa mkatili kiasi kile.
Lakini bila shaka ilikuwa ni
wakati ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi na
hasa baada ya kujifunza
maarifa haya ya utambuzi.
Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa
nasafiri kutokea Dar es salaam
kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar
es salaam saa 12.30 jioni.
Wakati ule mabasi yalikuwa
yakisafiri jioni na usiku, sio
kama siku hizi. Nilikuwa
ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya
ajira, nikiwa ndio kwanza
nimemaliza kidato cha nne.
Niliajiriwa moja kwa moja
serikalini, kwani siku zile ajira
zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa na kazi
niliyokuwa nafanya, hivyo
niliomba kazi kwenye kampuni
moja kule Arusha na niliitwa
kwa usaili. Tulifika mji
unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio
mji maarufu kwa hoteli zake
katika barabara yote ya Segera
hadi Moshi na Arusha.
Tulipofika Korogwe basi letu
lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia
kwenye hoteli moja ambayo
nakumbuka hadi leo kwamba
ilikuwa ikiitwa Bamboo.
Niliagiza chakula na kula
haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na
wenye basi la TTBS ambalo
ndilo nililosafiri nalo.Wakati wa
kulipa ndipo niliposhangaa na
kuogopa. Niliingiza mkono
mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza
kubabaika na mwenye hoteli
alisema hawezi kukubali ujinga
huo, "Abiria wengine wahuni
bwana, anakula na kujifanya
kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye hoteli
alisema kwa kudhamiria hasa.
Kulizuka zogo kubwa, huku
mwenye hoteli akisema ni
lazima anipeleke polisi. Ni
kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo
cha polisi ili nishughulikiwe.
Hapo Hotelini kulikuwa na
bwana mmoja aliyekuwa
amekaa pembeni na mkewe na
watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma
mhudumu mmoja aniite.
Niliondoka pale kaunta
nilipokuwa nabembeleza na
kuja kwa yule bwana. Alikuwa
ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama
50 hivi. Nilimsalimia na
aliitikia, nilimsalimia mkewe
pia. Yule bwana aliniuliza kisa
cha vurugu ile na nilimsimulia.
Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili
wakati nimeibiwa fedha zote
na ningerudi vipi Dar.
Nilimwambia nilikuwa
napanga namna ya kurudi Dar,
kama huko polisi ningeaminika. Kama mzaha vile yule bwana
aliniambia kuwa angenipa
fedha za kutumia huko Arusha
na nikirudi Dar nimrudishie
fedha zake. Nakumbuka alinipa
shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha
zake ofisini kwake.
Alinielekeza ofisini kwake,
mtaa wa Nkuruma na
kuniambia kuwa ameamua
kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji msaada wa
mwingine na maisha haya ni
mzunguko. Nilimshukuru na
kuondoka kukimbilia basini.
Basi lilikuwa linanisubiri mimi
tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole.
Tuliondoka Korogwe, lakini
haikuchukua muda basi letu
lilipata tatizo la pancha ya
gurudumu moja la mbele. Ilibidi
tuegeshe pembeni ili litengenezwe. Baada ya
matengenezo, tuliondoka
kuendelea na safari yetu.
Karibu na mji wa Same kwenye
saa saba usiku, basi letu
lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na
kulizuka aina ya kusukumana.
Huko nje kulikuwa na ajali.
Abiria tulishuka haraka na
wengine huko chini
walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka
niliona gari ndogo nyeusi ikiwa
imebondeka sana na hapo
kando kulikuwa na maiti
wawili. Nilijua ni maiti kwa
sababu walikuwa wamefunikwa
gubigubi. Halafu kulikuwa na
katoto kalikokuwa kanalia
sana kakiwa kamefungwa
kanga kichwani. Tumwahishe
huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa sio
sana. Nilikatazama kale katoto
ka kiume kenye umri wa miaka
kama mitatu. alikuwa
ameumia kwenye paji la uso,
lakini kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa ni wazazi
wake, kalikuwa yatima tayari.
Machozi yalinitoka. Baada ya
kupata msaada na
askari wa usalama barabarani
kuchukua maiti wale tulipanda basini kuendelea na safari yetu.
Kale katoto kalichukuliwa na
jamaa fulani waliokuwa na
Land Rover ya serikali
kukimbizwa hospitalini. Ndani
ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi
tunafika Arusha. Tulichelewa
sana kufika Arusha kwani
tulifika kwenye saa tano
asubuhi, badala ya saa mbili .
Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni
hiyo kesho, baada ya usaili
niliponunua gazeti ambapo
nilipata mshtuko mkubwa
ajabu. Kumbe wale watu
wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa ni yule
bwana aliyenisaidia hela na
mkewe. Yule mtoto wao ndiye
aliyeokoka. Niligundua hilo
baada ya kusoma jina lake na
jina la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi
Dar, pamoja na picha yake, mke
na mtoto. Nililia sana, kama
mtoto. Nillishindwa kujua ni
kwa nini
afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule?
Yalikuwa ni maswali yasiyo na
majibu na pengine maswali ya
kijinga pia.Nilijua kwamba
nilikuwa na deni, deni la
shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi tisini zilikuwa ni sawa
na shilingi laki moja za
sasa.Kwa mara ya kwanza sasa
nilijiuliza ni kwa nini
marehemu yule aliniamini
nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu. Nilikata kipande
kile cha gazeti
la kingereza kilichokuwa na
habari ile. Nilichukuwa kipande
hicho na kukiweka kwenye
Diary yangu. Deni, Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta
nikipiga magoti na kuomba
mungu anipe uwezo wa kuja
kulilipa deni la mtu yule
mwema kwa njia yoyote.
'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa
sura na namna ujuavyo wewe.
Nataka kulilipa deni hili ili nami
niwe nimemfanyia jambo
marehemu,' niliomba. Nilirejea
Dar siku hiyo hiyo.Kwa sababu ya mambo mengi na hasa
baada ya matokeo ya usaili ule
kuwa mbaya kwangu, nilijikuta
nikiwa na mambo mengi na
kusahau haraka sana kuhusu
mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa hata
hivyo kupata nafasi ya kusoma
Chuo cha Saruji na baadae chuo
cha ufundi na hatimaye
nilibahatika kwenda nchini
Uingereza. Mwaka 1991 nilianza shughuli zangu.
Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa
ofisini kwangu pale lilipokuwa
jengo Nasaco ambalo liliungua
mwaka 1996, ambapo
lilijengwa upya na kubadilishwa jina na kuitwa
Water Front. Nikiwa nafanya
kazi zangu niliambiwa na
sekratari wangu kwamba
kulikuwa na kijana aliyekuwa
anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui.
Nilimwambia amruhusu aingie.
Kijana huyo aliingia ofisini.
Alikuwa ni kijana mdogo wa
umri miaka kama 17 au 18 hivi,
mweupe mrefu kidogo. Alikuwa amevaa bora liende ,
yaani hovyohovyo huku afya
yake ikiwa hairidhishi sana.
Nilimkaribisha ilimradi basi tu,
kwani niliona atanipotezea
bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa
mtu mwenye huruma sana na
nilikuwa naamini sana katika
watu wenye pesa au majina.
Nilimuuliza, "nikusaidie nini
kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina kikao
baada ya muda mfupi".
Nilisema na sikuwa na kikao
chochote , lakini nilitaka tu
aondoke haraka. "Samahani
mzee, nilikuwa na shida...nimefukuzwa shule na
sina tena mtu wakunisaidia
kwa
sababu ...nime..niko ..kidato cha
pili na hivyo tu natafuta tu
kama atatokea mtu....Nilimkat isha. "Sikiliza kijana. Kama
huna jambo lingine la kusema,
ni bora ukaniacha nifanye kazi.
Hivi unafikiri kama nikiamua
kumsaidia kila mtu
aliyefukuzwa shule si nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda
Wizara ya Elimu
waambie..Kwanza wazazi
wako wanafanya kitu gani,
kwa nini washindwe ...Kwa
nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezo,
wanataka sifa?" "Hapana
wazazi wangu
walikufa na ninasoma shule ya
serikali. Nimekosa mahitaji ya
msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro,
Morogoro. Shangazi ndiye
anayenisomesha, naye ana
kansa na hivi sasa hata kazi
hafanyi..," Alianza kulia.
Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na
matumizi, kwa nini nisiwe
mwema, angalau kwa mara
moja tu. "Baba na mama
walifariki lini?" Niliuliza nikijua
kwamba, watakuwa wamekufa kwa ukimwi,
maana kipindi kile ndipo
fasheni ya ukimwi ilipoanza,
ambapo kila anayekufa
huhesabiwa kwamba kafa kwa
ukimwi. "Walikufa kwa ajali nilipokuwa
mdogo sana, nilipokuwa na
miaka mitatu. Ndio shangazi
yangu akanichukua na kunilea
hadi sasa anakufa kwa kansa."
Yule kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji
unayesoma hapa kwamba,
kuna nguvu fulani na sasa
naamini kwamba ziko nyingi
ambazo huwa zinaongoza
maisha yetu bila sisi kujua. Kitu fulani kilinipiga akilini
paaa! Nilijikuta namuuliza yuel
kijana. "Kwa nini umeamua
kuja kwangu, ni nani
alikuelekeza hapa na wazazi
wako walikufa mwaka gani na wapi?"Yule kijana alisema,
"Nimeona nijaribu tu kwa mtu
yeyote ambaye anaweza
kunisaidia, na ndio nimejikuta
nikiingia hapa, sijui....sikutu
mwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko
Same na mimi wanasema
nilikuwa kwenye ajali,
nikaokoka. Niliumia tu hapa."
Alishika kwenye kovu juu ya
paji lake la uso. Nilihisi kitu fulani kikipanda
tumboni na kuja kifuani halafi
niliona kama vile nimebanwa
na kushindwa kupumua. "Baba
yako alikuwa anaitwa nani?"
"Alikuwa anaitwa Siame..Cosmas Siame.."
Niliinuka ghafla hadi yule
kijana alishtuka . Nilikwenda
kwenye kabati langu mle
ofisini na kuchakura kwenye
droo moja na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka, nilitoa
kipande cha gazeti ndani ya
diary hiyo, nilichokuwa
nimekihifadhi. "Ndio alikuwa
anaitwa Cosmas
Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika."
Nilinong'ona. Nilijikuta nikipiga
magoti na kusali. "Mungu,
wewe ni mweza na hakuna
kinachokushinda. Nimeamini
baba kwamba kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya
kesho na kesho hiyo huanzia
hapa duniani." Halafu
nillinyamaza na kulia sana.
Nililia kwa furaha na ugunduzi
wa nguvu zinazomgusa binadamu kwa kila analofanya.
Nilisimama nikiwa
nimesawajika kabisa. Nilihisi
kuwa mtu mwingine kabisa.
Nilimfuata yule kijana na
kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia. "Mimi ni baba
yako mdogo, ndiye
nitakyekulea sasa. Ni zamu
yangu sasa kukulea hadi
mwisho" Naye alilia bila kujua
sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa.
Nilirudi kwenye kiti na
kumsimulia kilichotokea miaka
17 iliyopita. Tuliondoka hapo na
kwenda
kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la maziwa
ambako alikuwa amepanga
chumba. Kutokana na hali yake
nilimhamishia kwangu, baada
ya kumsimulia kilichotokea.
Huyo dada yake Cosmas alifurahi sana hadi akashindwa
kuzungumza kwa saa nzima.
Alifariki hata hivyo mwaka
mmoja baadae, lakini akiwa
ameridhika sana. Kijana Siame
alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na hivi
sasa yuko nchini Australia
anakofanya kazi. Ukweli ni
kwamba ni mwanangu kabisa
sasa. Naamini huko waliko
Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile
walichokipanda miaka mingi
sana nyuma. Lakini nami
najiuliza bado. Ilikuwaje
Cosmas akanipa msaada ule?
Halafu najiuliza ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame hadi
ofisini kwangu akizipita ofisi
nyingine zote? Nataka
nikuambie, usiwe mbishi sana
bila sababu, kuna nguvu za
ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu....NGUVU HIZO
NI UPENDO WA MUNGU! "
**MWISHO**

Author

Written by DK

Napenda kusafiri, hasa kutembelea kila mkoa katika nchi yangu nzuri Tanzania, nafanya hivyo maana hiyo ndio njia niliyochukua katika kutumikia taaluma yangu ya habari na mawasiliano ya umma

0 comments: