Japan kujenga reli iliyobomolewa na mafuriko Morogoro

Makamu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mitsuya Norio (Kushoto), akiwa na Naibu waziri wa uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, wakati walipotembelea miundombinu ya reli jijini Dsm jana.
 
Serikali ya Japan imeahidi kukarabati kipande cha reli kinachosumbua mara kwa mara kilichoko kati ya Kilosa na Dodoma.
 
Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Uchukuzi Dk. Charles Tizeba, wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Norio Mitsuya, aliyetembelea bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya reli (TRL) kujionea uendeshaji.
 
Ziara hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, alizotoa wakati wa ziara ya Afrika ili kuisaidia sekta ya miundombinu.

Alisema baada ya waziri huyo kujionea shughuli mbalimbali, kwa niaba ya serikali yake ameahidi kuisaidia Tanzania kuimarisha reli na bandari.
 
Aliongeza kuwa juzi kampuni hodhi ya miundombinu ya reli (Rahco) na TRL zilifanya tathmini ya eneo la Kilosa hadi Dodoma ambapo serikali hiyo iliahidi kulikarabati.

Aliongeza kuwa, baada ya ukarabati huo Japan itasaidia kuitengeneza rasmi ambapo gharama yake itajulikana pale tathmini itakapofanyika. Alisema nia ya kuisaidia Tanzania kwenye usafiri wa reli ni ya muda mrefu na kwamba kwa sasa wanatimiza ahadi hiyo.
 
Kuhusu bandari ya Dar es Salaam, alisema Japan itaipanua kwa kutengeneza gati namba moja hadi saba. Waziri Mitsuya alisema lengo la ziara hiyo ni kuisaidia Tanzania katika kuboresha miundombinu kwa siku zijazo.
 
Awali, Waziri Tizeba alisema kuwa, vichwa 13 vya treni ambavyo wameviagiza nchini Marekani hivi karibuni vinatarajia kuingia mwishoni mwa mwaka huu. Aliongeza vichwa hivyo vinagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 50.

Katika ziara hiyo, waziri wa Japan alipata nafasi ya kusafiri na treni ya Dar es Salaam kutoka stesheni hadi Ubungo.
 
CHANZO: NIPASHE

Author

Written by DK

Napenda kusafiri, hasa kutembelea kila mkoa katika nchi yangu nzuri Tanzania, nafanya hivyo maana hiyo ndio njia niliyochukua katika kutumikia taaluma yangu ya habari na mawasiliano ya umma

0 comments: