Shirika la Usafiri Dar (UDA) sasa kupangiwa `ruti`
Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (Uda) ambayo imebinafsishwa, wakati wowote kuanzia sasa itapangiwa ‘ruti’
kama zilivyo daladala nyingine.
Kwa kipindi kirefu mabasi ya Uda yameachwa kusafirisha abiria popote
yapendako bila kuzuiliwa hatua iliyolalamikiwa na baadhi ya wenye
daladala kuwa haiadhibiwi kwani ni mali ya vigogo.
Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra), David Mziray, alifahamisha kuwa magari hayo yatapangiwa
maeneo ya kutoa huduma kwa kuzingatia sehemu zenye upungufu wa mabasi ya
abiria.
Alisema yatapewa ruti katika kipindi cha wiki mbili zijazo kuanzia sasa,
akitaja baadhi ya sehemu zitakazofaidika na Uda kuwa ni pamoja na
Kigamboni, Kimara na Tegeta.
Aliongeza kuwa magari hayo hayatachorwa mistari na kupakwa rangi kama
zilivyo daladala nyingine bali yatakuwa na vibao sehemu ya mbele
kuonyesha eneo zinapoelekea.
Baadhi ya madereva wa daladala waliozungumza na gazeti hili walilalamika
kuwa Uda husafiri maeneo yasiyo na foleni na yenye abiria wengi mfano
Ubungo- Buguruni, Mwenge- Buguruni, Mbezi- Ubungo na wakati wote
zinakwepa foleni na ruti ndefu.
Akijibu malalamiko ya baadhi ya madereva wa daladala kuwa mabasi ya Uda
hayakamatwi na trafiki, Mziray alipinga.
“Baadhi ya madereva wa Uda wameshakutwa na makosa na kulipishwa faini,
makosa hayo ni kutoza nauli kubwa tofauti na ile iliyopangwa, pia
wamekuwa wakikatisha ruti na kutoa maneno machafu,” alisema.
Uda ambayo awali ilikuwa shirika la umma na mabasi yake kubandikwa namba
za ‘SU’ ilikuwa inamilikiwa na Shirika la Maendeleo la Mkoa wa Dar es
Salaam (DDC).
Hata hivyo, imeuzwa kwa wawekezaji binafsi na kuanza kushindana na
daladala kwenye sekta ya usafirishaji jijini hapa.
Akiwazungumzia madereva na utingo wa daladala wasiovaa sare, alisema
“ndiyo maana tunataka ifike mahali, mabasi yanayotoa huduma yawe ya
kampuni ili iwe rahisi kwetu kufikisha malalamiko kwa wahusika na hatua
za kinidhamu na kisheria kuchukuliwa dhidi ya kampuni inayohusika,”
alisema.
0 comments: