Nawasalimu nyote kwa jina la uzalendo na utaifa
uliotukuka, leo katika mwendelezo wa kampeni ya #DerevaMakini ambayo inalenga
kuishirikisha jamii katika kukabiliana na ajali ambazo zimekuwa mwiba kwa taifa,
nitaangazia wajibu wa taasisi, makampuni na watu binafsi katika kupunguza ajali
hizo.
Katika makala ya awali nilitaja orodha ndefu ya
wadau wanaohusika moja kwa moja kwenye sekta ya usafiri ambao wakitekeleza sawasawa
majukumu yao ajali zinaweza kupungua kama sio kukoma kabisa. Hivyo leo nitaanza
na makampuni ya simu za mkononi.
Mchango wa makampuni ya simu za mkononi katika
maendeleo ya sekta ya mawasiliano na uchumi kwa taifa ni mkubwa sana, lakini
pamoja na manufaa hayo bado kuna madhara makubwa yanayotokana na matumizi mabaya
ya simu za mkononi kwa madereva wakati wakiendesha magari yao.
Kwa mujibu wa Mtandao wa DailyMaily, takwimu
zinaonyesha kuwa Dereva mmoja (1) kati ya wanne (4) wanaotumia simu zao za
mkononi huku wakiendesha magari yao hupata ajali zenye ukubwa na madhara mbalimbali.
Hapa
ndio swali langu linapoibuka; Je, Makampuni ya simu zamikononi yamejiwekea
mikakati gani kuelimisha wateja wake juu ya madhara ya matumizi ya simu wakati
wakiendesha? Au wanachojali wao ni kutengeneza faida tu pasipo kuangalia
madhara yanayowakumba wateja wao?
Tumeona
ushiriki wa baadhi ya makampuni hayo katika wiki za nenda kwa usalama yakihimiza
usalama barabarani, lakini ingefaa zaidi kama ushiriki wao ungekuwa endelevu,
pengine wangeweka hata jumbe kwenye kadi za muda wa maongezi ili kila anayenunua
muda huo aweza kupata elimu Fulani.
Sote
ni mashahidi kwa makampuni yanayouza vileo, sheria inayalazimisha kuweka onyo juu
yamadhara yanayoweza kumpata mtumiaji endapo atatumia bidhaa hizo vibaya, jambo
ambalo linawezwa kuigwa na makampuni ya
simu nayo yakaanza kutoa onyo la matumizi mabaya ya simu kwa madereva
wanapoendesha.
Ni mtazamo tu, na wewe msomaji kupitia forum hii unaweza
kutupia mawazo, mtazamo, ushauri na hata maswali yako ukizingatia mada aliyetajwa
hapo juu, maoni yako tutayatumia kwenye mada ifuatayo.
Wiki ijayo tutaendelea kuwaangalia wadau wengine
na majukumu yao wakiwemo Askari wa Usalama Barabarani, Madereva, Abiria,
Wamiliki wa vyombo vya usafiri, Sumatra, Vyombo vya habari, Tanroads, Miundombinu
, TBS, Wauzaji wa magari, Sheli za mafuta na vipuli vya magari.
Kampeni hii ya #DerevaMakini inayolenga kupunguza
ajali za barabarani ikijikita zaidi kwenye mabasi ya abiria imewezeshwa na Michuzi
Blog, Tabianchi Blog na Transevents Marketing
Kwa taarifa zaidi tembelea Dereva
Makini
0 comments: