Nauli za mabasi mikoani zapanda, Kamanda wa trafiki atoa onyo kali

Wakati Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, likitangaza kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki na madereva wa mabasi yaendayo mikoani watakaobainika kupandisha nauli kiholela kipindi cha sikukuu, baadhi yao wamekiuka agizo hilo.
Kauli ya kuwachukulia hatua wamiliki na madereva wanaovunja sheria hizo za usafiri barabarani ilitolewa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani, Mohamed Mpinga, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana kuhusu mikakati yao ya kudhibiti ajali katika kipindi hiki cha sikukuu ya Krismasi na mwisho wa mwaka.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), nauli ya Dar es Salaam na Arusha zinatofautiana kutokana na viwango vya ubora kuanzia wa chini, Sh. 22,700, kati Sh. 32,800 na juu Sh. 36,000.

Akizungumza na NIPASHE, abiria wa basi la Sai Baba linalofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, Lameck Mushi, alisema alipofika katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo (UBT), alisema nauli ilikuwa Sh. 20,000, lakini  aliambiwa na mawakala kuwa nauli hiyo iliongezeka hadi  Sh. 25,000.

Kiwango hicho cha nauli ni kutoka Dar es Salaam hadi Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Abiria mwingine, Prisca Sabato, aliyesafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Mbeya, alisema alipofika katika kituo hicho cha mabasi Ubungo alidhani nauli ilikuwa ni Sh. 30,000, lakini aliambiwa na wakala kulipa Sh. 40,000.

Alisema nauli hizo zimekuwa zikiongezeka kutokana na ubora wa gari, hivyo katika safari moja wengine wanalipa nauli hadi Sh. 50,000 na wanapoulizwa wakatishaji tiketi huwajibu kuwa hiyo ni biashara huria.

NIPASHE ilifuatilia nauli za mikoa ya Mwanza na Geita ambayo kwa kipindi hiki pia idadi ya abiria inaongezeka na kuzungumza  na baadhi yao, lakini hawakuwa tayari kutaja majina yao.

Hata hivyo, walisema nauli imeongezeka kutoka Dar es Salaam hadi Geita na kufikia kati ya Sh. 50,000 na 60,000 kwa baadhi ya mabasi badala ya nauli ya awali ya Sh. 42,000.

Ofisa Leseni wa Sumatra, Sebastian Lohay, alisema wako tayari kutoa maelekezo kwa wamiliki wa mabasi ili wasikiuke sheria na taratibu zilizowekwa na kwamba wataichukulia hatua za kisheria kampuni itakayokiuka sheria hizo.

Aidha, kutolewa kwa taarifa hiyo ya Kamanda Mpinga, kunafuatia ajali za mfululizo zilizojitokeza ndani ya mwezi huu ambazo zimesababisha vifo vya watu wengi pamoja na majeruhi.

Ajali hizo ni pamoja na ile ya basi la kampuni ya Burudan, iliyotokea Kwalaguru, Barabara ya Chalinze-Segera, Tanga, hivi karibuni na kuua watu 12 na wengine 76 kujeruhiwa.

Ndani ya kipindi hicho hicho pia, ajali nyingine ilitokea eneo la Segera mkoani humo na kusababisha vifo vya watu wanane na 17 kujeruhiwa huku ile ya Longido, Arusha ikiua watu sita na kujeruhi wawili.

Pia ndani ya mwezi huu kulitokea ajali nyingine Ihumwa, Dodoma, baada ya basi la Simiyu Express, kuua watu wawili na kujeruhi 14 na kwamba vyanzo vya ajali hizo ni mwendo kasi.

“Wakati tunapoelekea katika sikukuu za mwaka, kuna mahitaji makubwa ya usafiri kwa abiria kwenda kuungana na familia zao kusherehekea pamoja. Kutokana na hili, baadhi ya watu hupendelea kutumia usafiri wao binafsi, lakini walio wengi wanategemea usafiri wa umma,” alisema  Kamanda Mpinga na kuongeza:

“Kwa wanaosafiri kwa usafiri wa umma, kuna mazoea ya kupandisha nauli kwa magari yanayokwenda sehemu mbalimbali zikiwamo kanda za hapa nchini.
Jeshi la Polisi linasema hii ni kinyume cha sheria na masharti ya leseni za usafirishaji yaliyotolewa na Sumatra. Hivyo Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kinawaasa wamiliki wa mabasi na mawakala wao wote kuhakikisha wanazingatia sheria hizi.”

Alitaka kila abiria apate tiketi inayoonyesha nauli sawa na kiwango alicholipa huku akiwaasa madereva kutowatumia wapigadebe au vishoka katika kupata abiria na kwamba magari yasiunganishe safari bila kufanyiwa huduma yanapotoka safari.

Sambamba na hilo, alisema katika kipindi hiki cha sikukuu na mwisho wa mwaka, jeshi hilo limejipanga kuongeza askari wake wa barabarani ili kudhibiti foleni ukiukwaji wa alama za usalama barabarani.

Aliongeza kuwa mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe, inaongoza kwa ajali ya magari yanayosafiri kwenda nje (Transit-IT), ambayo hayapaswi kuwa na abiria, kwani tangu Januari hadi Novemba, mwaka huu, watu 47 walifariki dunia na 83 kujeruhiwa.

Author

Written by DK

Napenda kusafiri, hasa kutembelea kila mkoa katika nchi yangu nzuri Tanzania, nafanya hivyo maana hiyo ndio njia niliyochukua katika kutumikia taaluma yangu ya habari na mawasiliano ya umma

0 comments: