Zikiwa zimebakia siku mbili kabla ya maadhimisho
ya sikukuu ya Krismasi, usafiri katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo
mikoani cha Ubungo jijini Dar es Salaam umeendelea kuwa mgumu kutokana
na nauli kupanda huku ukiwapo uhaba wa mabasi.
Kwa sasa nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi mikoa ya kaskazini ya Kilimanjaro na Arusha ni kati ya Sh. 50,000 na 70,000 huku waaendao Iringa na Mbeya wakilipa Sh. 22,000 kutoka 18,000.
Hata hivyo, NIPASHE imegundua kuwapo kwa baadhi ya magari madogo (Coaster) ambayo yanapakia abiria nje ya kituo katika maeneo ya Mbezi na Mwenge.
Akilizungumzia suala hilo, Kamishna wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Masumbuko Masuke, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa changamoto hiyo ni kubwa.
“Sumatra tayari imekwishaanza kushuhulikia tatizo hilo kwa kuweka kizuizi kipya cha Msata, mkoani Pwani kukagua ili kuhakikisha usalama wa magari hayo yanayopakia nje ya kituo,” alisema Masuke.
Katika hali ya kushangaza, baadhi ya abiria wamekuwa wakikwamisha zoezi la Sumatra la kuzuia ulipaji nauli wa zaidi ya kiwango stahili kwa kutoa kiwango kikubwa cha fedha ili kupatiwa tiketi. Jambo hilo lilijitokeza jana wakati Sumatra wakikagua moja ya mabasi yaendayo mikoani baada ya abiria mmoja iliyesema ukweli wa nauli aliyolipa na kunusurika kupigwa na abiria wenzake.
Hata hivyo, baada ya maofisa wa Sumatra walipoamuru abiria huyo arudishiwe kiasi kilichozidi, abiria wenzake walichanga na kumpa.
Mpaka NIPASHE inaondoka kituoni hapo, bado kulikuwapo msongamano mkubwa wa abiria waendao mikoa mbalimbali. Hata abiria waliokuwa wanakwenda mikoa ya jirani ikiwamo Dodoma leo na kesho kutokea Dar es Salaam, walilazimika kufanya booking jana.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments: