Abiria waliokwama na treni Dodoma wakisubiri mabasi kwa ajili ya usafiri wa kuelekea kwenye mikoa ya Morogoro na Dar es saalam ambapo shirika la Reli limewakodia mabasi kutokana na kushindwa kuendelea na safari kutokana na Mafuriko Gulwe na Godegode wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Abiria hao wakiwa hawajui la kufanya kutokana na kukosa chakula katika stesheni ya reli mkoani Dodoma walipotangaziwa kuanza kusafirishwa kwa mabasi lakini mpaka kufikia leo jioni zaidi ya abiria 900 kati ya 1600 walikuwa bado hawajapatiwa usafiri huo.
Mfanyakazi wa shirika Reli kituo cha Dodoma akibandika tangazo katika ubao wa matangazo lililowataka abiria waliokuwa wanaelekea mikoa ya kanda ya ziwa kurudishiwa nauli zao kutokana na usafiri wa treni kusitishwa kwa muda usiojulikana.
Askari wa kuzuia Ghasia (FFU) wakiangalia usalama kwa abiria wa treni waliokwama kutokana na treni kushindwa kuendelea na safari tangu juzi mara baada ya kufika kituo cha reli mkoani Dodoma kutokana na mvua iliofunika reli wilayani Mpwapwa.
Na John Banda, Dodoma
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRL) limelazimika kuwapakia kwenye mabasi abiria wake waliokwama kwa siku mbili katika Stesheni mkoani Dodoma waliokuwa wanasafiri kwa Treni kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, kutokana na kushindikana kwa ukarabati unaoendelea kufanyika mpaka sasa ambao umeonekana kushindikana kutokana na wingi wa maji yaliyopo kwenye eneo hilo la Gulwe na Godegode lililopo Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Stesheni hii Masta wa Kituo cha Reli Dodoma, Zakaria Kilombele alisema kuwa kutokana na hali hiyo ya ukarabati huo unaoendela kwa hivi sasa kwenye njia hiyo ya relishirika limeamua kuwasafisha abiria hao waliokwama kwa kutumia mabasi.
Kilombele alisema abiria hao waliokwama kwa siku mbili toka wafike kutoka mikoa ya Kigoma,Tabora na Singida na Mwanza mkoani hapa,jumla yao wamefikia 1800 na Shirika limewakodishia mabasi yapatayo 24, mpaka kufikia leo abiria wote watakuwa wamesafirishwa na
mabasi hayo yaliyokondishwa na shirika. “Mpaka sasa tayari abiria wapatao 935 wameshaondoka na ninategemea hawa wengine waliobaki mpaka kufikia leo jioni ni matarajio yangu watakuwa wamesafirishwa, kwa kuwa ninategemea kuletewa mabasi yapatayo tisa “alisema Kilombele.
Akizungumza kuhusu ukarabati unaoendelea kwenye eneo hilo korofi la
Gulwe na Godegode alisema mpaka jana alasili hali ilikuwa nzuri na tuliruhusu gari la abiria kuendelea na safari, lakini ilipofika majira ya saa 12 jioni maji yalianza kujaa kwenye eneo hilo na ikalazimika abiria hao kurudishwa stesheni ya Dodoma mjini.
Hata hivyo wakizungumza baadhi ya abiria hao walidai kuwa shirika hilo kitendo cha kuendelea kuwachelewesha juu ya safari kuna hatari ya kuwepo milipuko wa magonjwa matumbo kutokana na abiria walio wengi kujisaidia hovyo na kusababisha kila sehemu kuwa na vinyesi.
Mawazo Elisha ambaye ni abiria alisema kwa siku mbili tulizokaa hapo stesheni karibu abiria wengi wamekuwa wanajisaidia kwenye mabehewa ya abiria ambayo yamekwama hapo stesheni na yale mabovu hali hiyo inatokana vyoo vilivyopo neo hili kujaa.
“Vyoo vilivyopo vyote vimejaa na tunalazimika abiria kujisaidia kwenye mabehewa ambapo uchafu huu umetapakaa kwenye mataruma ya reli,hali ambayo imekuwa ikileta harufu kali katika eneo hilo”alisema Mawazo.
Naye Joshua Lazaro alisema shirika kuendelea kuwaweka katika eneo hilo limesababisha biashara zao kama vile samaki wameanza kuharibika na kuanza kutoa harufu na wadudu wa aina ya funza.
Alisema miongoni mwa abiria wamesafirisha biashara zao kama hao samaki na dangaa kwa maana hiyo hivi sasa wameanza kuharibika na kutuletea hasara kubwa ambayo hatufahamu nani watahusika.
Hata hivyo abiria walikuwa wameishakata tiketi kuelekea mikoa ya kanda ya ziwa walitangaziwa kurudishiwa nauli zao kutokana na mkanganyiko huo wa usafiri kwa njia hiyo ya reli uliojitokeza na mkuu huyo wa stesheni mkoa alisema hakutakuwepo na usafiri kwa muda usiojuilikana.
Mapema wiki hii jumla ya abiria wapatao 1600 waliokuwa wametoka mikoa ya Kigoma,Tabora Mwanza na Singina waliokuwa wamesafiri kwa usafiri wa reli walikwama stesheni ya Dodoma mjini na kuwalazimu kufanya maandamano hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Rehema Nchimbi kwa lengo la kutaka kuwapatia usafiri mwingine.
0 comments: