Rufiji: Siku moja baada ya ajali kuua watu 12 wilayani Same, ajali nyingine mbili mbaya zilizohusisha magari matano zimetokea katika eneo moja wilayani Rufiji na kuua watu 22, akiwamo kondakta wa gari aina ya Toyota Hiace ambaye kichwa chake kimetenganishwa na kiwiliwili.
Ajali hizo zilizopishana kwa dakika chache
zilitokea juzi saa 1:00 jioni katika Kitongoji cha Mkupuka, Kata ya
Kibiti na zilisababisha vifo vingi kutokana na watu 14 waliojeruhiwa
katika ajali ya kwanza iliyoua watu saba, kukanyagwa na gari jingine
wakati wakisubiri kupandishwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser la
Idara ya Maliasili ili kupelekwa hospitali.
Habari kutoka Kituo cha Afya cha Ikwiriri
zinaeleza kuwa miili ya watu wawili ilitenganishwa kichwa na kiwiliwili,
maiti tano zilikuwa na vichwa vilivyopasuka na maiti nyingine zilikuwa
zimekatikakatika mifupa.
“Hii ni ajali mbaya kati ya ajali ambazo nimewahi
kuziona maishani,” alisema mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Frank
Sixmund Mlangira (30) ambaye amelazwa Hospitali ya Mchukwi na ambaye ni
dereva wa gari aina ya Toyota Land Cruiser la Idara ya Maliasili ambalo
liligongwa katika ajali ya pili wakati likichukua majeruhi kuwapeleka
hospitalini. “Dereva wa Hiace alikatwa kichwa na kikatenganishwa na
kiwiliwili.”
Ajali ilivyokuwa
Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali ya kwanza ilitokea
wakati gari ya abiria aina ya Toyota Hiace lilipojaribu kukwepa lori
lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara na badala yake kugongana uso
kwa uso na lori aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likielekea Dar es
Salaam.
Katika ajali hiyo ya kwanza watu saba walikufa papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa.
Wakati juhudi zikifanyika kuokoa majeruhi na kutoa
miili ya waliofariki, basi jingine lililokuwa kwenye mwendokasi
likitokea Lindi kwenda Dar es Salaam, liliwakanyaga majeruhi 14
waliokuwa wakisubiri msaada na baadaye kugonga gari la Idara ya
Maliasili lililokuwa likipakia majeruhi kuwapeleka hospitali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema dereva mmoja anashikiliwa na polisi wilayani hapa kwa mahojiano.
Kamanda Matei alisema kuwa maiti 19 zimehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Ikwiriri na wawili wapo Kituo cha Afya Kibiti.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mchukwi, Dk. Zakaria
Lukeba alisema walipokea majeruhi 13 wa ajali hiyo na kuongeza kuwa kati
ya majeruhi hao, wawili walithibitika kuwa walishafariki kabla ya
kufika na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 23, idadi ambayo
inatofautiana na takwimu za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ambazo
zinaonyesha waliofariki eneo la tukio ni 21. Jana mchana majeruhi mmoja
alifariki na idadi ya waliofariki kufikia 22.
Alisema majeruhi watano wamehamishiwa Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi na kuongeza kuwa majeruhi sita tu
ndio waliobaki hospitalini hapo wakiendelea na matibabu.
Dereva wa gari la Idara ya Maliasili, Frank Sixmund Mlangira
alisema huenda dereva wa gari la Mining Nice alidhani alikuwa
anasimamishwa na majambazi ndiyo maana alikaidi amri ya kusimamishwa.
“Alionekana anahangaika akionekana kuamini kabisa magari yaliyokuwa
yamesimama yalikuwa yametekwa,” alisema Mlangira ambaye alijeruhiwa
kichwani.
Miili yahifadhiwa
Jeshi la Polisi lilitoa majina ya maiti
zilizohifadhiwa katika Kituo cha Ikwiriri kuwa ni za Nassoro Mohamedi
Kajani (20) mkazi wa Ikwiriri, Sikitu Ali Mpanga (32), Juma Saidi
Kitambulio (20) wa Mbagala, Salumu Juma (50) wa Charambe Mbagala,
Shabani Bakari (30) ambaye alikuwa kondakta wa Hiace mkazi wa Kibiti,
Ustaadh Kalilambwe wa Mbagala.
Wengine ni Shafii Kite (30) wa Mbagala Dar es
Salaam, Masudi Abilali (27) wa Mkuranga, Amini Mpemba (30) wa Jaribu
Mpakani, Ali Saidi(21) wa Kimanzichana, Japheti Posiani (24) wa Dar es
Salaam, Mwasabi Sabiri (45) wa Mbagala, Madadi Hassani Magosongo (45) wa
Jaribu Mpakani, Ramadhani Ali wa Mbagala, Abdalah Yusufu wa Mbagala,
Fikiri Saidi Sanze wa Vikindu Mkuranga, Selemani Mcharazi (47) wa
Mbagala, Hassani Wasabi (18) ambaye hafahamika wapi anatoka na maiti
mbili za watu waliofahamika kwa jina moja moja la Mostafa na Nyari.
Juzi, waombolezaji 12 waliopewa lifti na gari aina
ya Pick-Up walifariki dunia baada ya kupata ajali mbaya iliyohusisha
magari matatu.
Wakati huo huo, watu wanane hawajulikani walipo
baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kwenda Utete kusukumwa na mawimbi
na kumwaga baharini abiria wote 16 waliokuwa wamepakia.
0 comments: