Habari
zilizotufikia punde zinaeleza kuwa kesho kutakuwa na mgomo wa madereva
wa daladala kwenye Manispaa ya Morogoro. Mgomo huo utazihusisha daladala
za maeneo yote ya manispaa ya Morogoro jambo ambalo litapelekea kuwepo kwa shida kubwa ya usafiri mjini hapa.
Sababu
za kufanya mgomo huo ni kupinga vitendo vya kukamatwa na kutozwa faini
kubwa vinavyofanya mara kwa mara na askari wa usalama barabarani.
Katibu
wa umoja wa daladala njia ya Kilakala, George John ameuambia mtandao
huu kuwa wamelazimika kupanga kufanya mgomo huo kutokana na kukithiri
kwa uonevu unaofanywa na askari wa usalama barabarani ambao wamekuwa
wakiwakamata mara kwa mara na kuwatoaza faini kubwa.
John
amesema mgomo huo utahusisha kuegesha magari na kuandamana na mabango
katika maeneo tofauti tofauti ya mji hii ni kutokana na ombi lao la
kufanya maandamano hadi kwa Mkuu wa Wilaya kutupiliwa mbali na Mkuu huyo
wa Wilaya kwa madai kuwa ametingwa na maandalizi ya kiongozi wa juu wa
Serikali ambaye atazulu mkoani humo hivi karibuni.
Mtandao wa Safarimoja
umemtafuta (simu) Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo ili kupata
kauli yake juu ya mgomo huo, "Mimi sina taarifa za mgomo huo lakini kama
wamepanga kugoma kwa sababu ya kuonewa na askari wa barabarani hilo ni
haki yao japo kwangu mimi siwezi kusapoti kwa kuwa jambo hilo
litawaumiza wananchi wa Manispaa yangu"
Nondo
anasema hakubaliani na askari wa barabarani kuwaonea madereva wa
daladala lakini pia akisisitiza kuwa hakubaliani pia na madereva kukiuka
taratibu na sheria za barabarani.
"Kama
kuna uonevu unafanywa na askari barabarani mimi sikubaliani nao na ni
haki ya madereva kugoma, lakini haiwezekani madereva wote wakaonewa
pengine wanakiuka sheria za barabarani, sasa kama unafanya makosa ni
lazima utapewa tu adhabu kwa kupigwa faini" anasema Nondo.
Safarimoja pia imezungumza pia na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, Faustine Shilongile
ambapo amekiri kupata taarifa ya mgomo huo na kwamba jeshi la polisi
halitalegeza uzi kwa kuwakamata na kuwatoza faini wale wote wanaokwenda
kinyume na utaratibu wa sharia za barabarani.
Amesema
mgomo hauwezi kupindua sheria na kwamba hauwatishi askari kuendelea
kusimamia sheria hizo ambazo mara nyingi zimekuwa zikikiukwa na madereva
wa daladala mkoani humo na kuanza kulalamika pale wanapokamatwa na
kupigwa faini.
"Ni
kweli nimepata taarifa za mgomo, na sisi tunasubiri hiyo kesho wagome
halafu tutachukua hatua stahiki maana hatuwezi kuteteleshwa na migomo
inayoshinikiza kuacha kusimamia sheria, wao kama wanafanya makosa
wategemee kukamatwa na kulipishwa faini hata kama ni mara sita kwa siku
moja" anasema Kamanda Shilongile
Faini ya kosa moja ni shilingi 30,000 kwa maana nyingine dereva kama atapatikana na makosa manne kwa siku atatakiwa kulipa shilingi 120,000 jambo ambalo madereva wanalipinga vikali.
Mtandao wa Safarimoja unatoa tahadhali kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro kujiandaa kwa lolote ili
kuweza kuwahi kazini na kufanikisha shughuli zako nyingine kwa kutumia
usafiri mwingine endapo kweli azma ya madereva hao wataitekeleza.
Unahabari ya mambo ya usafiri? tuma kupitia safarimojatz@gmail.com
0 comments: