Bandari sasa kutoa huduma saa 24

Meli ikishusha mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Mamlaka ya Bandari Tanzania na wadau wake kuanzia sasa wataanza kufanya kazi saa 24

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na wadau wake, kuanzia sasa wataanza kufanya kazi kila siku kwa mwaka mzima ili kuongeza ufanisi ikiwa ni utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
 
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka alisema hayo jana wakati wa utiaji saini makubaliano kati ya wizara hiyo, TPA na wadau mbalimbali.
 
Mwanjika alisema lengo la mkataba huo ni kuhakikisha TPA kwa kushirikiana na wadau wote, wanafanya kazi kwa saa 24, siku saba za wiki kwa mwaka bila kupumzika.
 
Miongoni mwa wadau 15 waliotiliana saini ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Wakala wa Forodha na Uondoshaji Shehena Tanzania (Taffa), Benki za NMB, CRDB na Chama cha Wenye Magari ya Mizigo (Tatoa).
 
Kabla ya mpango huo, bandari imekuwa ikifanya kazi kwa saa 24 kwenye maeneo muhimu, lakini wadau wamekuwa wakifanya kazi kwa muda wanaojipangia wenyewe hivyo kukwamisha baadhi ya kazi.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande alisema kila mdau atatakiwa kutekeleza wajibu wake kama mkakati wa kufikia malengo ya mpango huo.
“Hivyo mdau yeyote asipotekeleza yaliyo kwenye mkataba, atakuwa amekwamisha mkakati mzima,” alisema Kipande.
wa kuboresha shughuli za bandari zetu,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Mwenyekiti wa Taffa, Steven Ngatunga alisema wizara hiyo itatakiwa kuwachukulia hatua wadau wasitekeleza wajibu wao.
“ Mizigo inapocheleweshwa kutolewa bandarini kuna wanaofaidi na kuna wanaoumia, hii ina maana wenye mizigo wanatozwa faini lakini kuna wadau wanaosababisha hilo hawatozwi faini, sasa hivi yoyote atakayechelewesha mizigo apewe adhabu,” alisema.
Ngatunga ambaye alitishia kutosaini mkataba huo kutokana na mapungufu yaliyopo, baadaye alisaini baada ya Katibu Mkuu kumweleza kuwa kila wakati kutakuwa na mabadiliko yenye lengo la kuboresha mpango huo.
Aliipongeza Serikali kuwa kuanzisha mpango huo wenye lengo ya kuboresha ufanisi katika bandari hiyo.
“Napongeza kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu licha ya kuchelewa kuanza kwa sababu nilishatoa ushauri miaka mingi iliyopita,” alisema.
Wadau wengi waliotia saini ni Mkemia wa Serikali, wizara ya Ujenzi, Wizara ya Kilimo na Chakula, Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Wakala wa Vipimo na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Wengine ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena Bandarini (Ticts).
Chanzo;Mwananchi

Author

Written by DK

Napenda kusafiri, hasa kutembelea kila mkoa katika nchi yangu nzuri Tanzania, nafanya hivyo maana hiyo ndio njia niliyochukua katika kutumikia taaluma yangu ya habari na mawasiliano ya umma

0 comments: